Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (MB), leo Agosti 6, 2026, amezindua rasmi Bodi ya Nne ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD), akiielekeza kuisimamia chuo kwa uongozi wenye maono, uwajibikaji na ubunifu ili iwe kitovu cha ubora katika elimu, tafiti na maendeleo ya jamii nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Gwajima amesema Bodi inaanza kazi katika kipindi muhimu cha mageuzi ya Taasisi baada ya kuunganishwa kwa vyuo vinane vya maendeleo ya jamii kuwa kampasi za TICD.
Amesisitiza Bodi isimamie utoaji wa elimu yenye ubora, iharakishe matumizi ya teknolojia za kidijitali, iimarishe tafiti zinazotoa suluhisho kwa changamoto za jamii na kuongeza ushindani wa Taasisi kitaifa na kimataifa ili kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. John Elton Lusingu, ameishukuru Serikali kwa imani iliyoiweka kwa Bodi hiyo na kuahidi kuwa wajumbe watafanya kazi kwa weledi, uadilifu na ushirikiano ili kutekeleza kikamilifu maelekezo yaliyotolewa na Serikali huku Mkuu wa Chuo, Prof. Bakari George, akisema kuwa Menejimenti ya TICD itaendelea kushirikiana kwa karibu na Bodi katika kutekeleza mipango na vipaumbele vya Taasisi kwa lengo la kuimarisha ubora wa elimu, tafiti na huduma kwa jamii.
Bodi ya Nne ya TICD inaundwa na Dkt. John Elton Lusingu (Mwenyekiti), Prof. Bakari George (Katibu), pamoja na wajumbe Dkt. Waheeda Shokat, Dkt. Alex Nkondola, Bi. Angelista E. Kihaga, Bw. Yasin Sanuku, Bw. Pendason Philomen, Bw. Bahati Ndoweka na Bw. Martin Mashaka.
Published: 22 Aug 2026